RIWAYA: MUAFAKA - 4




RIWAYA: MUAFAKA
MTUNZI: Amri BAWJI
SEHEMU YA NNE
“Sawa iwapo unadhani hivyo. Lakini watu wanasema ‘vichwa viwili ni bora kuliko kimoja.’’
“Kama ni hivyo basi niwache nifikirie peke yangu, nitakapojiona ninahitaji msaada wa mtu mwengine nitakwambia wewe Edo unisaidie.”
“Tafadhali usiwache kufanya hivyo Lulu. Pale unapoona ninaweza kusaidia, basi wakati wowote, saa yeyote, pahali popote nieleze nitakuwa tayari kusaidia.’’
“Natanguliza shukrani, Ahsante Edo.’’ Lulu alianza kupendezewa na mazungumzo kati yake na Edo. Yalikuwa yakimfarijii na kumliwaza. Mazungumzo kati yao yalikuwa rahisi yasiyokuwa na majivuno wala kujitapa. Hali kama hiyo iliendelea kwa muda kiasi kumfanya Lulu aanze kuvutika taratibu kwa Edo.
* * *
Hisia za Vicky juu ya Onespot zilifika kiwango ambacho alishindwa kujikaza kwa kukaa kimya na kuonesha ishara kuwa anampenda kijana huyo. Aliamua asema kwa namna moja au nyingine huku damu ikimwenda mbio mwilini mwake Vicky alitamka kumuuliza Onespot aliekuwa amekaa juu ya kiti kikubwa nyuma ya meza yake ya ofisi.
“Onespot , leo jioni unakwenda wapi?’’
Onespot alinyanyua uso wake kumuangalia Vicky kwa sura ya kushangaa.
“Siendi popote Vicky, kwani vipi unataka kunialika?!’’
“Hapana, ninataka wewe unialike mimi…Onespot.’’
“Hapana shaka Vicky, why not?! Sema ungependa kwenda wapi? Ni nani ambaye asingependa kutoka na msichana mrembo kama wewe mtoto wa mzee Kapate?!’’ Kama kawaida yake Onespot ni mtu wa maneno mengi na majisifu aliendelea kusema,
“Lakini utani mbali Vicky, mimi na wewe tukiwa pamoja! We make a good pair au sio?” Kwa Onespot ilikuwa faghari, kwa wasichana wengi waliowahi kuanza hata kumtongoza yeye kwanza, kabla hajawaambia lolote, na kwa Vicky ingawa upo wakati alitamani amtoe nje kwa matembezi, lakini pia zilikuwa zinakuja hisia za u-dada dada, kwa vile baba zao ni marafiki wakubwa.
Vicky moyo ulizidi kumwenda mbio akajiona kama yupo kwenye ndoto, aliitikia swali la mwisho la Onespot kwa kutamka.
“Ndio…ndio…we make a good pair.’’
“Nadhani watu wakituona watazimia,…kama tunatoka sayari nyingine vile. Sio utani Vicky mimi na wewe wazuri bwanaa!’’
Jioni ile Onespot alimtoa Vicky nje, walipata chakula cha jioni ndani ya hoteli moja kubwa na maarufu jijini Dar es salaam. Kisha wakatembelea majumba ya starehe kwa muziki na vinywaji Vicky alivuta hatua ya kwanza aliyokuwa anaiwania.
Uhusiano wa Lulu na Edo uliweza kuzaa penzi. Zipo baadhi ya siku waliweza hata kutembelea maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam pamoja, baada ya saa za kazi. Edo alijikuta kuwa hawezi kupitisha siku pasipo kumuona Lulu. Mapenzi hayajifichi, kwa namna walivyokuwa, kila mmoja hapo kazini alijua kuwa Edo na Lulu wapo mapenzini, habari ambayo iliweza kumfikia Onespot ambae hakuipokea kwa furaha. Vile vile baada ya kufanya uchunguzi wake, aliona wazi kuwa Edo na Lulu wanapendana.
* * *
Onespot kwa anavyoamini yeye, ni kuwa hakuna msichana ambae anaweza kumkataa. Bado maishani kwake kumuona msichana anaemtaka yeye, akakataa. Alilolizowea ni kutakiwa yeye kwanza na wasichana kama vile alivyoanzwa na Vicky. Suala la kuangushwa na Lulu kila alipomtaka awe nae pamoja, lilimvuruga akili yake, zaidi ya yote ni Lulu kumkubali mwanamme mwingine pale pale kazini… Kazi anayomiliki mwenyewe. Siku moja alimuita Lulu ofisini kwake. Lulu wakati anaingia ofisini kwa Onespot alisikia sauti ikimkaribisha kwa upole, ilikuwa sauti ya Onespot.
“Karibu… karibu princess Lulu”. Wakati anamkaribisha hivyo, Onespot alikuwa ameipa mgongo meza yake na anaangalia kiwambazani. Lulu alisogea mbele ya meza, na kusema,
“Ahsante Onespot!” Bila kugeuka, Onespot aliendelea kuangalia ukutani.
“Karibu ukae Lulu”.
“Ähsante.” Lulu aliketi juu ya kiti taratibu na kuwaza moyoni mwake vipi huyu!!!. Onespot alizunguka na kiti chake kwa ghafla na kutamka. “Enhe, Lulu ni lini mimi na wewe tutatoka nje pamoja kwa ajili ya matembezi?” Lulu alimuangalia Onespot kwa kiasi cha nukta chache bila kusema chochote. Kisha akakukumbuka kuwa yeye na Onespot kwa siku ile, walikuwa bado hawajaonana, kwa hiyo, ni kwamba bado hata hawajasalimiana. Lulu alipewa ujumbe tu kuwa anahitajiwa ofisini kwa boss Onespot, ghafla alitamka kusalimu,
“Habari za asubuhi Onespot?”
“Hujasikia swali nililokuuliza?”
“Habari za asubuhi Onespot?” Lulu nae alirudia tena kumsalim Onespot huku uso ameukunja kiasi cha kumfanya boss huyo atabasamu kidogo na tayari alihisi kuwa kama hatamuitikia Lulu, hawawezi kufika mbali katika maongezi anayoyahitaji, aliamua kuitikia.
“Habari za asubuhi nzuri tu Lulu, je, wewe hujambo?”
“Sijambo”.
“Je, sasa umeridhika? Yaani huwezi kujibu swali la mtu yeyote kabla ya kusalimiana?”
“Ndivyo nilivyofunzwa, ndivyo nilivyolelewa, kusalimu kwanza unapokutana na mtu na ndio uungwana.”
“All right… Ok, sasa jibu swali langu.”
“Swali lako lipi?”
“Lini tutatoka nje pamoja?”
“Kwenda wapi? Na kwa ajili gani?”
“Kwenda ni popote utakapo chagua wewe na ni kwa ajili ya mimi na wewe kuwa pamoja, peke yetu… ili uwe wangu binafsi.” Lulu alitoa tabasamu la dharau
kidogo likiambatana na mguno.
“Kwanza ni kuwa sina nitakapopachagua, pili, sipendi kuwa na wewe peke yetu nje ya ofisi hii kwa suala lisilokuwa la kikazi na mwisho sitaki niwe wako binafsi.” Alitamka maneno haya kwa taratibu na sauti ya chini yenye msisitizo.
Onespot aliposikia hayo, alicheka kidogo, kisha nae akamwambia Lulu,
“Hivi Lulu unaweza kuniambia ni sababu gani unanikataa?!”
“Sina sababu zozote sitaki tu”
“Hapana… hapana ni lazima ziwepo sababu, kwani kwa uanaume anaohitaji msichana yeyote, mimi kwako nimekamilika, ninazo pesa, ni mzuri wa sura na umbo, ni msafi, ninajua kujitunza, ninajua kuvaa na mwisho kabisa ninakupenda, sasa lipi linalokufanya unikatae Lulu?!!!”
Lulu aliinamisha kichwa chake chini akifikiria amjibu nini Onespot, mwisho alirudisha pumzi kwa nguvu na kumtazama mvulana huyo.
“Sikiliza Onespot, hayo yoote uliyosema, ni yako wewe.. ni kwa upande wako, pendo ni lazima liwe pande zote mbili… mimi… mimi… sikupendi.”
“Unampenda nani?!” Lulu, lilikuwa swali gumu kwake, pamoja na kuwa alijuwa wazi anampenda Edward kwa wakati huo, lakini hakuwa tayari kulitangaza pendo lake.
“Simpendi mtu yeyote.” Alijibu kwa sauti isiyokuwa na uhakika.
“Kwahiyo jaribu kunifikiria, naamini itakuwa rahisi kunipenda mimi kwani hakuna msichana asiethubutu kufanya hivyo kwangu.” Onespot alisema kama kawaida yake kwa kujiamini kabisa.
“Sitaki kukupa matumaini, lakini siwezi kukupenda Onespot pamoja na sifa zako zote. Ninahisi sifa hizo ulizonazo, ndizo zinazonifanya nisiweze kukupenda.” Onespot alisimama toka kitini alipokuwa amekaa kwa ghafla na kugonga meza yake kwa ngumi ya mkono wa kulia kwa nguvu.
“Shit! Kwanini huniambii kwamba unampenda Edo na ndio maana unanikatalia ombi langu.” Nae Lulu alisimama kwa hasira na kusema,
“Kumbe unajua ninampenda Edo, sasa kwanini unapoteza muda wako pamoja na wangu pasipo maana!!” Onespot aliondoka nyuma ya meza alipokuwa amesimama na kwenda mbele ya meza aliposimama Lulu. Alimshika mkono wake na kumgeuza asimame sawa sawa na kumuelekea yeye Onespot.
“Tazama”. Alijionesha yeye mwenyewe kwa kujielekeza viganja vyake vya mikono yote miwili kuanzia juu ya uso wake hadi chini nyayoni.
“Nitazame vizuri, labda siku zote hizi unaniangalia kwa woga. I am rich, handsome and all… I am one and only, one… spot. Huwezi kunikataa mimi kwa ajili ya yule tapeli. Una bahati sana kupendwa na mimi Lulu. Kwahiyo ninakupa nafasi ya mwisho, iwapo utagundua utapeli wa huyo Edo wako unaweza ukarudi kwangu nitakupokea. Usihofu, Edo is a lier and a womaniser!”. (Edo ni muongo na asharati)
Wakati Onespot anamaliza kusema maneno haya, Lulu tayari yupo mlangoni anatoka.
* * *
Onespot alisimama hapo alipokuwa kwa muda usiopungua dakika tano, kisha taratibu akaondoka kuelekea kwenye kiti chake nyuma ya meza kubwa ya ofisi. Aliketi na kuegemea kiti hicho kwa nguvu uso wake ukiwa umeelekea juu. Halafu alikunja mikono yake miwili juu ya meza, kisha akaiwekea paji lake la uso juu yake. Alianza kufikiri, yeye Onespot, mtoto wa James Pato, aliyejaliwa kuwa na kila kitu kizuri mwanamme anachohitaji kuwa nacho ulimwenguni humu, kwanini asimpate msichana huyu mmoja Lulu, japo kwa kutoka nae nje siku moja tu !! Alijaribu kutafakari je ni kweli anampenda Lulu?! Hakuweza kupata jibu sahihi moyoni mwake
wala akilini mwake. Lakini hata hivyo aliwaza, awe anampenda Lulu au hampendi, ukweli ni kuwa Lulu ni mrembo, na yeye Onespot amemtaka msichana huyo ingawa aonekane nae tu. Kwanini Lulu akakataa?!! Kwanini? … Kwanini? Onespot alinyanyua uso wake ghafla na akanyanyua mkono wa chombo cha simu uliokuwa kulia kwake hapo juu ya meza.
“Haloo?… nani Vicky?… Tafadhali tuma mtu akaniitie Edo… Mr. Edward Oloi… aje hapa ofisini kwangu sasa hivi ikiwezekana… eeh ndio… fanya haraka please!” Aliutua mkono wa simu kwenye chombo chake, kisha nae akaegemea tena kiti chake kwa nguvu. Akaiangalia dari ya chumba hicho cha ofisi. Akafumba macho yake kujaribu kufikiria tena. Wakati huu alimuwaza Vicky. Alipojaribu kuwalinganisha wasichana wawili Vicky na Lulu katika mawazo yake, alitambua kuwa wote ni warembo. Alipofikiria ukweli wa hisia zao, alikubali na moyo wake kuwa Vicky anampenda yeye Onespot kweli kweli. Pia akagundua kwamba na yeye moyo wake haumkatai Vicky kama anavyoonekana. Lakini ni kwanini Lulu amkatalie analolitaka yeye?!! Sauti ya kugongwa kwa mlango wa ofisini kwake ghafla ilimtoa kwenye mawazo aliyokuwa nayo na akafunua macho yake kuangalia mlango unaogongwa.
“Karibuuh!” Aliitikia kwa sauti ya juu lakini ya uchovu. Edo alijitokeza na uso wenye tabasamu kubwa,
“Habari za asubuhi Onespot?!”
“Nzuri tu, karibu ukae kitini”. Onespot alimuitikia na kumkaribisha Edo bila uchangamfu, jambo lililomfanya Edo ahisi kuna jambo na akanywea kidogo.
“Äsante Onespot!” Aliketi taratibu huku akimuangalia huyo boss wake kwa makini.
“Nilichokuitia hapa Edo ni kukuuliza ni kitu gani kinachoendelea kati yako na Lulu?” Edo alitoa tabasamu kidogo kisha akajikohoza na kuanza kusema,
“Tumekwisha maliza kupiga ile filamu ndogo ya tangazo la sabuni ya kuogea ya Kiu. Leo nilikuwa namalizia kuifanyia editing. Tumepanga na mwenzangu Bwana Rama Sele, kesho au keshokutwa tuanzae ku-shoot tangazo la magodoro ambalo litamuhusisha bwana Halfan Di na Lulu vile vile. Kwa hivi sasa hizi ndizo shughuli tulizonazo mkononi zinazohusu mimi na Lulu!”
Onespot alimuangalia Edo kwa jicho la kuua na kumuambia,
“Edo, mimi sifanyi dhihaka hapa, I am serious. Ninakuuliza kuhusu wewe na Lulu, habari zenu binafsi, sio habari za kazi… usijifanye hukunielewa bwanaa!!”Alisema kwa sauti ya kukasirika na huku uso kaukunja.
“Ni kweli kabisa niamini Onespot”. Edo alijibu kwa sauti ndogo na kuendelea kusema, “Kama ndiyo hivyo, basi sikukuelewa. Nilidhani unaniuliza habari za kazi zinazohusu mimi na Lulu”.
“Sasa umekwisha nielewa, haya nijibu!”
“Kinachoendelea kati ya mimi na Lulu, kibinafsi! Umekwisha tamka ni ki-binafsi! kwahiyo hakihusiani na ofisi hii.” Edo alijaribu kujikaza wakati anatamka haya, kwani tayari alikwisha hisi harufu mbaya ya panya wa kuoza ndani ya mazungumzo ya Onespot.
“Mimi kama boss wenu nyinyi nyote wawili, wewe na Lulu, ninataka kujua.” Onespot alisisitiza kwa kutumia uajiri wake.
“Kuwa mimi na Lulu, wewe ndie boss wetu, hilo silikatai, nakubaliana nawe. Lakini kwa suala langu binafsi, ni langu, siwajibiki kwa mtu yeyote hapa kazini.”
“ Sawa, wewe ni mjuaji, haya tuyafupishe mazungumzo. Sasa nijibu wewe na Lulu mnapendana?”
“Niulize hivi je, mimi ninampenda Lulu?!”
“Kama ndivyo unavyotaka kuulizwa haya jibu”.
“Ndio ninampenda Lulu. Tena sanaa!”
“Kama ndivyo hivyo basi mimi pia ninampenda Lulu bwana Edo.”
“Sawa endelea kumpenda, lakini ufahamu kuwa kumpenda kwako, hakutanizuia mimi kumpenda pia bwana Onespot.”
“Na wewe pia ufahamu bwana Edo, tutakuwa wawili sisi, tunawania kitu kimoja!”
“Sio suala la kuwania, Onespot! Mimi nimekwisha pata.” Onespot alitabasamu kidogo alipomuambia haya Edo.
“Kwanini useme hivyo?!!Hujaoa bwanaa, aliyepata ni aliekwishaoa.”
“Na iwapo tunao mpango huo wa kuoana?!”Edo alimuuliza Onespot kwa sauti ya chini. “Nitamgombea Lulu sitamuachia kirahisi nami ninao uwezo wa kila hali… kumbe hunijui mimi Edo?!” Alisema kwa maringo na bila kuonesha hofu yeyote.
“Ninakujua kuliko unavyojijua wewe mwenyewe… ni wewe ndie ambae hunijui mimi?”
Edo nae kwa wakati huu aliamua kumuondolea hofu kabisa kijana mwenzie huyo.
“Wewe unanijua vipi Edo?!
“Ninakujua ni kijana ulievimba kichwa kwa sababu ya utajiri wa baba yako. Ni kijana unaedhania unacho kila kitu kuliko vijana wenzako wote duniani. Ni kijana unayejidanganya kuwa hakuna msichana anaeweza kukukataa wewe. Ni kijana ambae pasipo utajiri wa baba yako, basi si lolote si chochote, hohehahe jungu la mavi na mkorogowe. Pasipo utajiri wa baba yako, usingejua hata barabara inavukwa vipi!” Onespot alibaki kumtolea macho Edo tu akimsikiliza anavyomsagia.
“Kumbe Edo u mzungumzaji mzuri sana, lakini yote hiyo ni sababu ya mapenzi na wivu.”
“Mapenzi!? Ndio sababu ya mapenzi ya Lulu. Je, wivu wa nani? Ni nani nimuonee wivu?!!
“Mimi, Onespot, unanionea wivu sababu ninacho kila kitu ambacho wewe ungependa uwe nacho. I have got everything that you would like to have.” Edo alisimama akaangua kicheko kikubwa kilichomfanya Onespot aduwae kidogo. Kisha akamnyooshea kidole Onespot kifuani kwake na kumuambia,
“Wewe, kwa taarifa yako Onespot mimi ni mtoto wa pekee wa wazazi wangu kama wewe. Wazazi wangu wanacho kila kitu ambacho wazazi wako wanacho na zaidi. Mimi pamoja na kujua kwamba rasilmali na pesa yote ya baba yangu ni yangu, lakini sipendi kuwa tegemezi, napenda kujihangaisha. Nimesoma na nimesomea napenda kupata ujuzi wa kuajiriwa na ndio maana niko hapa kwenye kampuni yako leo. Sifanyii shida, nafanyia hoby na kupata ujuzi zaidi wa kazi niifanyayo.” Wakati wote huu Edo alikuwa anatamba ofisini kwa Onespot kwa kuenda huku na kurudi huku. Alisimama na kumuangalia Onespot kwa dakika chache kisha akasema,
“La mwisho Onespot, sikuonei wivu, sababu Lulu ananipenda mimi na hakupendi wewe… kwaheri.” Wakati Edo anaanza kuondoka, Onespot alimsimamisha,
“Subiri Edo.” Edo aligeuka na kumuangalia Onespot ambae alisema
“Yote uliyosema hata yakiwa ni kweli lakini… Lulu bado hajakuwa wako.”
“Tutaonana… Onespot!”
“Tutaonana Edo, hakuna msichana, anaeweza kusema ‘Hapana’ kama mimi Onespot ninamtaka.” Edo alimuangalia kwa jicho la dharau na kutabasamu kidogo. Onespot aliendelea kusema,
“Kwa asili mimi Onespot nimezaliwa ‘mshindi’ kwahiyo siwezi kushindwa na vita ndogo kama hii ya kumpata msichana kama Lulu.”
“Fahamu mkataa kushindwa si mshindani. Ni kweli Onespot umezaliwa ‘mshindi’ kwa asili, lakini kwa hakika si ‘mpiganaji’. Wewe ni mshindi katika vita vilivyokwisha piganwa na wenzio!”
ITAENDELEA KESHO ASUBUHI!!!!
TOA MAONI YAKO!!

Comments

Popular posts from this blog

Chombezo : Huruma Ya Dudu Sehemu Ya : Pili (2)

Leyla binti bikra -01

Chombezo: mwajamu utamu sehemu ya 15 (mwishoo)