RIWAYA: MUAFAKA - 5
MTUNZI: Amri Bawji
SEHEMU YA TANO
“Tutaonana Edo, hakuna msichana, anaeweza kusema ‘Hapana’ kama mimi Onespot ninamtaka.” Edo alimuangalia kwa jicho la dharau na kutabasamu kidogo. Onespot aliendelea kusema,
“Kwa asili mimi Onespot nimezaliwa ‘mshindi’ kwahiyo siwezi kushindwa na vita ndogo kama hii ya kumpata msichana kama Lulu.”
“Fahamu mkataa kushindwa si mshindani. Ni kweli Onespot umezaliwa ‘mshindi’ kwa asili, lakini kwa hakika si ‘mpiganaji’. Wewe ni mshindi katika vita vilivyokwisha piganwa na wenzio!”
“Hivi vita vya kumgombania Lulu, nitapigana mwenyewe, na ndio maana sitaki hata kukufukuza kazi ili nikutowe ‘knockout’ bwana Edo.” Kama kawaida ya Onespot, pamoja na udhaifu wote aliokuwa nao, lakini alikuwa ni mtu mwenye kujiamini kupita kiasi,
“Kunifukuza kazi huwezi bwana Onespot kutokana na mikataba yetu, bali ninaweza niache kazi mwenyewe nikitaka kufanya hivyo. Lakini na mimi sitaki kuwacha kazi sababu ninataka nione ni jinsi gani unaweza kumgombania Lulu dhidi yangu mimi.”
“Sio kama ninampenda sana Lulu, la hasha, isipokuwa kuanzia sasa, nitahakikisha ninakushinda, ili nawe usimpate. Ndipo utakapofahamu bwana Edo kuwa mimi ni mpiganaji vile vile si mshindi wa asili tu.” Ëdo alimtazama Onespot kwa makini na kusema,
“Sikiliza maneno yangu Onespot, hata mimi narudia tena hata mimi pia ni ‘mshindi’wa asili, lakini ninapenda kupigana vita mwenyewe. Ninacho kila kitu mvulana anachohitaji kuwa nacho katika maisha yake, huko nyumbani ninakotoka… pamoja na msichana wa kumuoa. Ninapenda kupigana vita vyangu, mwenyewe.” Onespot alijichekesha kicheko cha chini chini na dharau tele. “Kama ndivyo hivyo, basi ni afadhali uanze kufikiria kumuoa huyo msichana uliewekewa huko nyumbani kwenu. Forget about Lulu, nitahakikisha hamuoani.” Edo alionekana kuchoshwa na kujiamini na kujitapa kwa Onespot. Hakutaka kuendeleza malumbano kati yake na huyo boss wake kijana. Aliondoka na kutoka ofisini hapo kwa Onespot.
Onespot alidhamiria kufanya alilomuambia Edo yaani kupigana vita mwenyewe vya kumgombania Lulu. Alitulia tuli alipoachwa na Edo, na kufikiria ni jinsi gani atapigana vita hivyo. Kwa dakika chache kichwa chake alijihisi kuwa ni kitupu, amesema kwa hasira tu, lakini ni vigumu kupigana dhidi ya mapenzi. Lulu anapendana na Edo, ni kwa vipi atalivunja pendo lao?!! Mapenzi ni kitu ambacho, watu wanasema mtu akiwa kweli yu mapenzini basi anaweza kufanya lolote, linalostahili na lisilostahili. Kwa hiyo atumie njia gani ili alisaliti penzi la Edo na Lulu?!! Mawazo yalimjia na kumkumbuka Vicky ambaye alifahamu wazi kwamba msichana huyu anampenda yeye Onespot. Aliamua kuwa dawa ya mtu ni mtu, na ibilisi wa mtu ni mtu, iwapo kweli Vicky anampenda yeye, basi atafanya lolote atakalo muambia alifanye. “Nitamtumia Vicky kuvunja penzi la Lulu na Edo” aliwaza na kusema kimoyo moyo.. Alipiga simu na kumuita Vicky wakati huo huo. Vicky pasipokupoteza dakika hata moja aliwacha alichokuwa akifanya na kuondoka kuelekea ofisini kwa boss Onespot ambaye alikuwa anapenda saa zote ikiwezekana amuone machoni mwake. Vicky alipoingia ofisini, Onespot alisimama kutoka kitini, nyuma ya meza alipokuwepo na kwenda mbele ya meza hiyo. Vicky alipofika karibu yake, pasipo kusema neno lolote alimvuta, akamgandamiza kifuani pake kwa kumzungushia mikono yake yote miwili mgongoni pake. Vicky alijihisi kuyeyuka hapo juu ya kifua cha Onespot huku moyo ukimuenda mbio kama farasi wa ujinini. Alijitahidi, nae akanyanyua mikono yake na kumkumbatia Onespot.
“Vicky?” Onespot alimuita kwa jina kwa sauti ndogo.
“Mhuu!” Nae Vicky aliitikia, muitiko wa mguno pasipo kutamka neno, kichwa chake akiwa amekiegemeza kwenye kifua cha Onespot.
“Do you love me?!” (Unanipenda?!)
“Ÿes, I do”(Ndio ninakupenda)…Na wewe pia unajua kuwa ninakupenda kweli.”
“Ninataka unihakikishie kwa matamshi yako Vicky.”
“Ninakupenda kweli Onespot kuliko ninavyoweza kutamka.” Onespot alizidi kumkumbatia Vicky na kubaki hivyo kiasi cha dakika kadhaa. Nae Vicky alitamani wabaki katika hali hiyo hiyo kwa siku hiyo yote. Alijihisi raha ya ajabu. Aliona sasa pendo lake halikupotea bure, limepokelewa ipasavyo. Lakini mara ikamjia hisia
katika moyo wake ya kutokukubali kikamilifu, kwani kama Onespot anampenda kama anavyompenda yeye, mbona bado hajatamka hivyo, ameulizwa yeye tu kama anampenda Onespot alinyanyua kichwa chake taratibu kutoka kifuani kwa Onespot na kumuangalia usoni.
“Önespot?!”
“Naam, unasemaje Vicky?!”
“Je na wewe unanipenda?”
“Usiulize jibu Vicky…ndio ninakupenda.”
“Unanipenda kiasi gani?”
“Kiasi cha kukutaka wewe uwe mke wangu… je, Vicky utakubali kuolewa na mimi?!”
Vicky hakuamini masikio yake. Alijiona kama yumo ndani ya ndoto. Pasipo kujitambua alijikuta machozi yakimtiririka toka macho yake ambayo aliyatuliza katika kumuangalia Onespot usoni. “Nimekubali Onespot, ndio nitakubali kuolewa na wewe.” Onespot alimnyanyua Vicky mikononi mwake na akaenda nae kwenye kochi kubwa lililokuwemo ndani ya ofisi hiyo huku akimuangalia machoni. Alimuweka juu ya kochi hilo nae akaketi karibu yake.
“Vicky, unafahamu watu wanaopendana huchukuana kwa raha na tabu?!
“Ndio, hilo nina lifahamu.”
“Na unajua kuwa kila binadamu anayo mambo yanayompa raha na yapo yanayompa tabu vile vile?”
“Hilo pia ninalifahamu Onespot.” Onespot alirudisha pumzi kwanza, na kuanza kufikiria aanze kusema vipi jambo alilolikusudia kulisema. Aliinamisha uso wake chini kisha akaunyanyua kumuangalia Vicky, halafu akarudia kuangalia chini kwa unyonge, kiasi akamtia Vicky wasiwasi.
“Mbona hivyo Onespot! Kwani kuna jambo gani linalokunyima raha?!”
“Ah, we acha tu.” Onespot alijibu hivyo kwa kujinyongesha kweli, lakini moyo wake ulikuwa ukichekelea kwa kuona amekwisha mfikisha Vicky alipopataka amfikishe.
“Niache vipi Onespot! Nawe ulikuwa ukisema sasa hivi hapa, kuwa kwa wapendanao huwa wanashirikiana raha na tabu! Kwa hiyo usihofu, tabu yako ndio yangu, niambie tu.” Uso wake ukionesha huzuni, alinyanyua viganja vyote viwili vya Vicky na kuvifumbata na viganja vya mikono yake, aliyaangalia macho ya msichana huyo na kusema,
“Sikiliza Vicky nisingependa kukuingiza katika mambo yasiyo ya muhimu, pamoja na kuwa jambo lenyewe linanikera kwa sababu ya jeuri niliyofanyiwa, lakini silioni kuwa ni la maana… hasa kwako.” Sauti ya kubembeleza ya Onespot ilimfanya Vicky ajibu,
“Madam hilo jambo linakukera, basi ni la muhimu, na sio kwako wewe tu, bali ni kwa sisi wawili sote, liseme usiogope.”
Onespot alifikishwa alipopataka hasa. Alisita sita kidogo kisha akaanza kusema,
“Vicky mpenzi wangu, usinielewe vibaya, haja yangu mimi kubwa, kutokana na jeuri niliyofanyiwa, ambayo sitakueleza sasa hivi, ni kuona urafiki wa Lulu na Edo unavunjika. Nataka unielewe, sina ubaya nao, bali nataka wasiwe pamoja kimapenzi. Na iwapo litafanikiwa jambo hilo, basi siku hiyo au inayofuata itakuwa ndio siku ya ndoa yetu mimi na wewe. Yaani wakiachana Edo na Lulu basi tutafunga ndoa mimi na wewe siku hiyo hiyo.” Vicky alitoa viganja vyake kutoka viganja vya Onespot taratibu huku kainamia chini.
“Vipi Vicky mbona umebadilika mara?!!”
“Hapana, sina hoja wala swali katika utashi wako wa kutaka kuona uhusiano wa Edo na Lulu unavunjika, lakini… lakini wasiwasi wangu ni kuwa kwa nini ndoa yetu itegemee kuvunjika kwa mapenzi yao?!”
“Ahaa, ngoja nikueleweshe ikiwa wasiwasi wako ndio huo. Ni hivi, ikiwa
nitafunga ndoa na wewe kabla hilo halijakuwa, nitakuwa sina raha kwa upande wangu. Na sababu nitakueleza baada ya hilo la kutengana kwa Edo na Lulu kutimia, kabla ya ndoa yetu.” Vicky aliona akiuliza mengi, anaweza amfanye Onespot abadilishe mawazo juu yake, wakati pendo lake ndio kwanza linachemka kiwango cha juu. Aliamua liwalo na liwe bora ataolewa tu na Onespot. ‘Hakuna cha rahisi kila kitu sharti ukipiganie siku hizi’ aliwaza. Kwa hiyo aliamua kumuunga mkono mpenzi wake Onespot kwa kutamka,
“Sawa… sasa umepanga kufanya nini?”
“Very good… vizuri sana Vicky.”Onespot alijibu kwa furaha na tabasamu. Alisimama na kutazama kando huku ameng’ata kidole cha shahada cha mkono wa kulia na mkono wa kushoto, amejishika kiuno. Alijifanya kama anafikiria nini la kufanya. Kisha akakaa tena juu ya kochi na kumshika mabega Vicky.
“Ninakuomba unisaidie kwa hili tu mpenzi wangu!”
“Sema tu ninakusikiliza.”
“Vicky, wewe ni mwanamke, na siku zote mwanamke anazo mbinu za kumfanya mwanamke mwenzake aone wivu. Kazi kwako Vicky, jifanye u mpenzi wa Edo, kwa Edo mwenyewe, na vile vile hakikisha Lulu ajuwe au ahisi kwamba lipo jambo linaendelea kati yako wewe na Edo. Nami nitakusaidia katika hilo kwa upande wangu, mimi, niachie Lulu, lazima nitambabaisha.” Onespot alimuangalia Vicky ambae alikuwa ametulia na kumuangalia kama vile kuruta anaesikiliza amri kutoka kwa mkuu wa kikosi jeshini. Aliendelea kusema,
“Usiwe na hofu Vicky, wakati wote huu tutakuwa tunakutana na kupanga mambo yetu kwa wakati wetu wenyewe. Kwa kuanza, nitaandaa onesho la mavazi mbalimbali na nitakutaka wewe uwe mwanamitindo katika onesho hilo. Kwa nini, jinsi gani, namna gani yote hayo niachie mimi. Ni lazima tushinde kusudio letu.”
* * *
Edo baada ya kuachana na Onespot, alikwenda moja kwa moja kumtafuta Lulu, alimkuta kwenye chumba cha wasichana. Alimuomba waonane mara moja, walitafuta sehemu faragha, wakaketi na kuzungumza. Edo akiwa katika hali ya kughadhibika bado, kutokana na mazungumzo kati yake na Onespot; alimuuliza Lulu,
“Hivi Lulu umewahi kukutana na Onespot leo?” Lulu alimuangalia Edo na kutabasamu kidogo. Hakutaka kumueleza yaliyomkuta yeye kwanza kwa hiyo aliuliza,
“Kwani kumetokea nini Edo?!”
“Hapana bwana, yule mtu kanivuruga akili yangu vibaya sana leo.”
“Amekufanya nini?” Lulu alimuuliza tena Edo kwa utaratibu.
“Eti ameniita ofisini kwake na kuniuliza kitu gani kinaendelea kati yetu sisi, yaani mimi na wewe. Mimi nikadhani anauliza kuhusu kazi, nikamueleza. Lakini kumbe anataka ajuwe uhusiano wetu binafsi. Tumekwaruzana hapoo, mwisho nikaona heri niondoke.” Lulu alicheka kidogo kwa jinsi alivyomuona Edo alivyohamaki kisha nae akamueleza kila kitu kilichotokea kati yake na Onespot asubuhi ya siku hiyo.
“Sasa Lulu, huyu bwana anatutafuta nini hasa.”
“Anasema ati na yeye ananipenda.”
“Na mimi pia ameniambia hivyo hivyo kuwa nae anakupenda pia.” Edo alisema huku amejiinamia, mwisho alisogea karibu sana na alipokuwa amekaa Lulu, alinyanyua viganja vya Lulu mikononi mwake kisha akapeleka vidole hivyo midomoni na kuvibusu. Halafu akamuangalia tena Lulu machoni mwake na kusema,
“Lulu, je upo tayari kuolewa na mimi?!” Lulu anampenda sana Edo, lakini katika akili zake bado ana wasiwasi na chaguo lake. Alifikiri ‘Je Edo ni mwanamme alie sawa kabisa kuwa mume wangu?! Je ataonekanaje mbele ya wazazi wangu?! Je sifa zake zinashinda za yule mchumba niliechaguliwa kule nyumbani?!’ Ilimradi maswali mengi yaliyojaa ndani ya kichwa chake, yalimfanya Lulu asiwe na jibu la haraka kwa swali aliloulizwa na Edo, ingawa, alifahamu fika kuwa kwa sasa yu mapenzini na Edo. Aliamua aombe muda kwanza wa kufikiria hivyo, akatamka, “Edo, tafadhali naomba unipe muda kidogo kwa swali lako hilo. Ninaomba usinielewe vibaya, kwani ni kweli ninakupenda, bali suala la ndoa, naomba muda kidogo wa kufikiria.”
“Nami pia nisingependa jibu la haraka haraka lisilokuwa na uhakika. Ninachotaka ufahamu ni kuwa nimekwisha kukuuliza swali hilo. Sasa nami nakuomba uchukue muda wa kunipa jawabu litokalo moyoni mwako.”
* * *
ITAENDELEA!!!
Comments
Post a Comment