.RIWAYA: MUAFAKA - 6



MTUNZI: AMRI BAWJI
SEHEMU YA SITA
“Lulu, je upo tayari kuolewa na mimi?!” Lulu anampenda sana Edo, lakini katika akili zake bado ana wasiwasi na chaguo lake. Alifikiri ‘Je Edo ni mwanamme alie sawa kabisa kuwa mume wangu?! Je ataonekanaje mbele ya wazazi wangu?! Je sifa zake zinashinda za yule mchumba niliechaguliwa kule nyumbani?!’ Ilimradi maswali mengi yaliyojaa ndani ya kichwa chake, yalimfanya Lulu asiwe na jibu la haraka kwa swali aliloulizwa na Edo, ingawa, alifahamu fika kuwa kwa sasa yu mapenzini na Edo. Aliamua aombe muda kwanza wa kufikiria hivyo, akatamka, “Edo, tafadhali naomba unipe muda kidogo kwa swali lako hilo. Ninaomba usinielewe vibaya, kwani ni kweli ninakupenda, bali suala la ndoa, naomba muda kidogo wa kufikiria.”
“Nami pia nisingependa jibu la haraka haraka lisilokuwa na uhakika. Ninachotaka ufahamu ni kuwa nimekwisha kukuuliza swali hilo. Sasa nami nakuomba uchukue muda wa kunipa jawabu litokalo moyoni mwako.”
* * *
lngawa Lulu na Edo wamezoeana, wanafanya kazi pamoja mpaka hatua ya kupendana hata kutaka waoane, lakini hakuna hata siku moja ambayo Lulu alimpeleka Edo nyumbani anakoishi kwa dada yake Flora na shemeji yake Abraham. Hata hivyo Lulu alikuwa mara moja moja anazizungumzia habari za Edo kwa muhtasari. Alitaka afanye jambo lililo kamili, alionelea wakati akifikia kumpeleka mvulana yeyote na kumjulisha kwa dada yake na shemeji yake, basi mvulana huyo awe tayari kufunga nae ndoa. Na kwa vile mara zote wanaume ndio wanaoanza kutongoza na kusema suala la kuingia kwenye ndoa, basi Lulu alisubiri nafasi hiyo itokee ndipo ampeleke Edo nyumbani anakoishi. Kwa hiyo alipoulizwa swali lakutaka yeye na Edo akubali waoane, pamoja na fikira zote, aliazimia kuwa afikapo nyumbani siku hiyo, amueleze habari hiyo dada yake. Hata hivyo swali hilo la Edo ingawa hakulijibu, lakini lilimrudishia furaha moyoni mwake ambayo ilitoweka baada ya mkutano wake yeye na Onespot uliofanyika asubuhi ya siku hiyo. Alimaliza shughuli alizokuwa anazifanya hapo kazini, kwa furaha baada ya kuachana na Edo. Lulu alikuwa kila dakika anaangalia saa yake ya mkono na kuomba kimoyo moyo muda uende haraka ili aweze kurudi nyumbani na kuonana na dada yake. Hatimae muda wa saa za kazi ulikwisha na kila mmoja akajitayarisha kuondoka. Lulu alikwenda kuagana na Edo, waliahidiana kuonana siku ifuatayo na ikiwezekana Lulu alishauri watoke kwa matembezi ya jioni siku hiyo, kisha wakaachana. Wakati Lulu yupo karibu na mlango wa mbele wa jengo la ofisi hiyo, alisikia sauti ya msichana ikimuita, aligeuka kutazama ni nani anaemuita, alikuwa ni Vicky. Lulu alitabasamu na kuuliza,
“Vipi Vicky, wasemaje?!” Vicky alitazama huku na huko kama vile anaemtafuta mtu vile, akamuuliza Lulu,
“Samahani Lulu, hivi hukumuona Edo hapa?”
“Nilikuwa nae dakika chache zilizopita, sasa sina hakika kuwa amekwisha toka au bado… kwani una shida nae?!” Vicky alikunja uso huku akiangalia saa yake mkononi na kurudia kutazama pande zote kwa wasi wasi,
“Ah! Tumeagana tukutane baada ya saa za kazi, tuna kijisafari kidogo tunataka tuende pamoja, sasa sijui yupo wapi! Edo bwana siku zote ukiahidiana nae sharti umtafute yeye. … Lakini haidhuru… basi Lulu… samahani… nitamfuata nyumbani kwake kama amekwishatoka.” Lulu alibaki ameduwaa, alijikokota taratibu na kuanza kuondoka kuelekea nyumbani kwao, hali ya kuwa furaha yake imekwisha pungua. Hilo lilikuwa pigo la kwanza.
Wakati Lulu anaingia nyumbani anakoishi alisikia sauti za vicheko vya watu zaidi ya wawili zilitokea sebuleni. Alisita kidogo na kuwaza kuna mgeni gani aliyekuja?! Maana nyumbani humu wanaishi watu watatu tu kwa sasa, yeye Lulu,
dada yake Flora na shemeji yake Abraham. “Sasa huyo mwengine ni nani?...Tena ni mwanamme.” Alinyanyua hatua ndogo ndogo kuelekea huko vicheko vilikokuwa vinatokea. Alipofika sebuleni aliduwaa kimya akiwa macho ameyatoa pasipo kuaamini. Mgeni na mtu wa tatu aliyekuwa akiongea na kucheka na Flora na Abraham, alikuwa si mwengine bali ni Onespot. Wote watatu waliangalia upande aliposimama Lulu, na wakasitisha vicheko vyao kidogo.
“Karibu… Karibu Lulu… Tupo hapa na Bwana Onespot Pato, ambae si mgeni kwako wewe kwa alivyotufahamisha yeye ndie Boss wenu.” Abraham alisema kwa furaha bila wasi wasi. Lulu alimuangalia Onespot kwa jicho la kuua, ambae nae alitabasamu na kusema,
“Nilitaka kukupa surprise visit Lulu.”
“Ulitaka au tayari umenipa?!!” Lulu alimuuliza, Onespot, nae alijibu,
“Usijali Lulu, surprise or no surprise, kwa jinsi mimi na wewe tulivyo, it is ok.” Lulu alionekana kukasirishwa mno na ugeni huo wa Onespot alimjibu kwa ghadhabu.
“Mimi na wewe tukoje?! Enhee niambie mimi na wewe tulivyo, tukoje zaidi ya kuwa muajiriwa na muajiri!?” Flora alikwisha hisi kuwa mdogo wake Lulu amekasirika kwa tendo la Onespot kuja kwao pasipo kualikwa, alimgeukia mdogo wake na kumwambia.
“Sikiliza Lulu, kama kuna jambo lolote kati yako na Onespot, liwe zuri au baya, sisi hatulijali. Tunachojali sasa hivi ni kuwa Onespot yumo ndani ya nyumba yetu na kwahiyo ni mgeni wetu. Siku zote kwa mila zetu za ki-Afrika mgeni anapewa heshima yake ya ugeni, awe ametaarifu au hakutaarifu kuja kwake. Tafadhali nakuomba. Usimfedhulikie Onespot.” Onespot alimuangalia Flora kwa jicho la shukrani na upole, kIsha akageuka kumtazama Lulu ambae bado alikuwa amesimama kwa tabasamu la ushindi.
“Sawa dada, samahani… mimi niko ndani chumbani kwangu…” Akasitishwa na sauti ya shemeji yake Abraham,
“Lulu, hebu tafadhali sahau angalau kwa saa hizi ambazo huyu bwana ni mgeni wetu, nakuomba urudi ujiunge na sisi hapa tulipo.” Lulu kusikia hivi alirudi taratibu na akaenda akakaa karibu na shemeji yake huyo, kama vile anahitaji hifadhi yake. Onespot alitabasamu huku akimuangalia Flora na kugeuza shingo na kumuangalia Abraham, kisha akasema kwa sauti ya kukata tamaa,
“Basi ni kama mnavyoona hali halisi ilivyo, bwana Abraham na Bi Flora, mimi na huyu bibie picha haziendi kabisa, sijui nimemtenda kisa gani. Natamani ningejua angalau nikamuomba msamaha.” Lulu alijisikia kama aliemeza jiwe, alihisi kipo kitu kikubwa kimemkwama kwenye kongomero la ndani ya shingo kiasi cha kumfanya ashindwe hata kusema neno lolote. Flora alimuambia Onespot kuwa maadam Lulu ni muajiriwa katika kampuni yake, basi anao ule wasiwasi na heshima kwa kufahamu Onespot ni bosi wake, lakini asimfikirie vibaya. Waliendelea kuzungumza hili na lile huku wakinywa soda. Onespot alijaribu kutumia uchangamfu wake wote na akafanikiwa kujenga imani ndani ya vichwa vya Flora na Abraham. Wakati wote huo Lulu alikuwa amekaa kimya kabisa kama vile hakuwepo. Mwisho kabisa Onespot alitamka,
“Najuta kwanini sikuifahamu au niseme hatukujuana na familia yenu mapema kabla ya leo. Kwani ni dhahiri kuwa nyinyi ni watu wacheshi na wazungumzaji wazuri.” Alimtulizia macho Lulu na kuendelea kusema,
“Una bahati sana Lulu… kuwa na familia kama hii uliyonayo” Lulu hata bila kumuangalia usoni alimjibu kwa mkato,
“Asante”. Onespot alitoa shukrani nyingi kwa Flora na Abraham na kuomba wawe wanakutana mara kwa mara na kupanga ni lini na wao watamtembelea kwao. Wao nao Abraham na Flora walimshukuru Onespot kwa kuwatembelea
na kumkaribisha tena siku nyingine anapopata nafasi. Waliagana na Onespot akaondoka. Lulu usiku huo hakupata usingizi mzuri. Furaha yote aliyokuwa nayo kwa kipindi kifupi cha alasiri ile hakuwa nayo tena. Kwanza suala la Vicky kumtafuta Edo lilimtatanisha akili yake, kila alivyojaribu kuliweka sawa hakuweza kupata ufumbuzi wake. Pili ilikuwaje Onespot kuja nyumbani kwao?! Alifuata nini?! Alizungumza nini na shemeji yake na dada yake kabla yeye hajawasili pale nyumbani?!!! Maswali mengi ambayo hakuweza kuyapatia majawabu, yalimchanganya akili yake. Aliomba usiku ule uishe upesi.
* * *
Siku iliyofuata, baada ya kazi Lulu alimfuata Edo na kumuomba watoke pamoja kama walivyoahidiana. Walitafuta Hotel iliyokuwa nzuri na kimya. Muziki wa sauti ya chini wa ala ukitumbuiza wateja. Walichagua meza iliyokuwepo pembeni mwa chumba cha kulia, wakakaa. Wakati wamekwishaagiza chakula alichochagua kila mmoja wao, waliendelea na kunywa vinywaji baridi taratibu. Ndipo Lulu alipomuuliza Edo,
“Vipi Edo, safari yenu wewe na Vicky jana ilikuwa nzuri?” Edo nusura apaliwe na juisi aliyokuwa akinywa aliposikia swali hilo. Alikohoa kidogo, akakunja uso katika kumuangalia Lulu usoni na kujibu kwa kuuliza,
“Safari?!!…; Mimi na Vicky?! Mbona sikuelewi Lulu?!” Lulu alitabasamu kidogo, akaendelea kunywa kinywaji chake ili ampe muda Edo aweze kukumbuka, lakini badala yake alionekana ni kweli halielewi swali la Lulu.
“Ina maana Edo, hukuenda hiyo safari au humjui Vicky?!”
“Vicky ninamfahamu vizuri, si yule katibu muhtasi wa Onespot?!”
“Ndie huyo huyoo!”
“Basi amini usiamini Lulu, sina safari niliyokwenda mimi na Vicky!!!”
“Lakini ulikuwa una ahadi naye ya kumpeleka pahali fulani?!”
“Hapana, ninakataa kabisa sikua na ahadi na yeye wala na mtu yeyote… Lakini Lulu wazo hili la kuwa mimi na Vicky tulikuwa na safari ulilipata wapi?!” Kwa wakati huo Edo alionekana amechanganyikiwa.
“Ämeniambia Vicky mwenyewe…, tena alisema kuwa kila mnapoahidiana kukutana, huwa unampa taabu, kwani ni lazima akutafute yeye!”
“Ni Vicky huyo aliesema hivyo?!”
“Ni yeye mwenyewe!” Edo alitoa pumzi kwa ishara ya kuchoka sana kwa habari anazoelezwa na kuulizwa.
“Lulu, ninaapa kwa jina la Mungu, sikuwa na ahadi na Vicky wala sijawahi kuenda nae popote hata siku moja, zaidi ya kuonana na kusalimiana tu, pale pale ofisini. Nipo tayari mimi na wewe tuende tukamuulize jambo hili kwa pamoja.” Lulu baada ya kumuona Edo jinsi alivyo na viapo anavyoapa, alimuamini na akamuambia,
“Basi haina haja ya kuenda kumsuta Vicky… maana itakuwa ni kusutana. Kama jambo lipo basi halitajificha litaonekana tu, na kama halipo, limepikwa tu, basi pia tutaona. Maadam umeapa, basi na tuliachie mbali na ninakuomba Edo tafadhali usimuulize Vicky kitu chochote. Tuone itakuwaje baada ya hapa.”
“Sawa Lulu, kama ndivyo upendavyo.”
Baada ya hapa chakula walichoagizia kililetwa, wakala na kuzungumza habari nyingine. Hatimae Edo alimsindikiza Lulu nyumbani kwao, bali hakuingia ndani ya nyumba hiyo.
* * *
Siku mbili baadae, Onespot aliitisha mkutano wa wafanyakazi wote wa kampuni yake. Aliwaeleza mipango yake ya kuandaa onesho la mavazi ya mitindo mbalimbali ya kike na ya kiume iliyobuniwa na wabunifu mahiri nchini. Aliwaambia anataka onesho hilo liwe kubwa naliweke historia, kwa hiyo maandalizi yake ambayo yatawahusisha wafanya kazi wote wa kampuni hiyo anataka yaanze mara moja baada ya mkutano huo.
“Watu wote.” Alisisitiza.
“Wawe wawajibikaji katika suala hili.” Alitulia kidogo na kumuangalia Vicky aliekuwa karibu yake na kumwambia,
“Hata wewe, Vicky ninataka uache hizo kazi zako za ukatibu na kuwa mwanamitindo kwa kipindi hiki. Lipo vazi ambalo tumejadili na wabunifu wamitindo, wameona kuwa wewe, litakupendeza zaidi. Umenielewa?” Alisema kwa sauti ya kuamrisha kidogo, nae Vicky akajidai kama vile jambo hilo ndio kwanza analisikia, akaitikia kwa kigugumizi,
“Nnnn… ndi.. nii.. nime… kuelewa boss” Huku sura yake ikionekana kutokuridhika na shauri hilo kumbe vile ni kuigiza tu mbele ya watu, lakini ni jambo analolijua, na limepangwa na Onespot pamoja na yeye. Watu wote waliokuwepo walibadilishana mawazo mbalimbali kuhusu agenda hiyo, mwisho mkutano ulivunjwa. Wakati watu wanatawanyika kutoka chumba cha mkutano, Onespot alimwita Edo,
“Bwana Edo, tafadhali tuonane ofisini kwangu.”
“Vema Onespot, nitakuja.” Baada ya muda mfupi Onespot alikutana na Edo ofisini kwake.
“Bwana Edo, ninachotaka kukuambia ni kuwa samahani sana kwa mazungumzo yetu kati ya mimi na wewe yaliyotokea hapa ofisini pangu juzi, let us forget about it, tuyaachilie mbali. Sasa hivi ninachotaka ni hii kazi tuliyotoka kuizungumzia mkutanoni ifanikiwe. Tufanye kazi bwana, mengine tuyatupilie mbali.” Onespot alizungumza haya, kwa taratibu na upole. Nae Edo akasema,
“Kazi ndio niliyoijia hapa ofisini pako, kwa hiyo nitaifanya kama itakikanavyo.”
“Very good, you are a gentleman, u muungwana bwana Edo, I like it, napenda hali kama hii.” Ghafla alionekana anamchangamkia Edo kwa maneno ya sifa na kumuamini.
“Wajua Edo, kuna hili vazi ambalo nimelijadili na mbunifu wake na kumtaka Vicky ashiriki kwa ajili ya vazi hilo, ninaomba tafadhali umsaidie sana huyu Vicky, kwani yeye si mwanamitindo kama wengine, hana uzoefu, kwa hiyo anahitaji ujuzi wako.” Edo alikumbuka mara ile ile maneno ya Lulu kuhusu Vicky na yeye. Alihisi upo uwezekano ikawa kuna mkono wa Onespot katika kusingiziwa kwenda safari yeye na Vicky. Lakini aliamua akubali ili aweze kugundua ukweli ulipo.
“Ujuzi wangu kama upi Onespot?!” Aliuliza.
“Wewe u mpiga picha mzoefu na mwenye ujuzi na umekwisha fanya kazi hiyo na wanamitindo wengi wenye uzoefu, kwa hiyo utamuonesha Vicky staili zitakikanazo. Picha zake tutazihitaji kwa ajili ya matangazo ya biashara vile vile. Jambo hili ni muhimu kwa faida ya kampuni.” “Una uhakika kuwa sio kwa faida yako binafsi bosi Onespot?!” Edo aliuliza kwa dhihaka huku kimoyomoyo akiwa ni kweli analouliza. Onespot alicheka kwa nguvu huku akitikisa kichwa kukataa,
“Hapana… hapana Edo… Oh no! sio kwa faida yangu binafsi… You must believe me Mr. Oloi.”
Edo alielezwa nguo hiyo ambayo ataivaa Vicky ni lini italetwa na mara ifikapo zoezi lianze.
* * *
ITAENDELEA!!!

Comments

Popular posts from this blog

Chombezo : Huruma Ya Dudu Sehemu Ya : Pili (2)

Leyla binti bikra -01

Chombezo: mwajamu utamu sehemu ya 15 (mwishoo)