RIWAYA: MUAFAKA - 7
MTUNZI: AMRI BAWJI
SEHEMU YA SABA
“Ujuzi wangu kama upi Onespot?!” Aliuliza.
“Wewe u mpiga picha mzoefu na mwenye ujuzi na umekwisha fanya kazi hiyo na wanamitindo wengi wenye uzoefu, kwa hiyo utamuonesha Vicky staili zitakikanazo. Picha zake tutazihitaji kwa ajili ya matangazo ya biashara vile vile. Jambo hili ni muhimu kwa faida ya kampuni.” “Una uhakika kuwa sio kwa faida yako binafsi bosi Onespot?!” Edo aliuliza kwa dhihaka huku kimoyomoyo akiwa ni kweli analouliza. Onespot alicheka kwa nguvu huku akitikisa kichwa kukataa,
“Hapana… hapana Edo… Oh no! sio kwa faida yangu binafsi… You must believe me Mr. Oloi.”
Edo alielezwa nguo hiyo ambayo ataivaa Vicky ni lini italetwa na mara ifikapo zoezi lianze.
* * *
Wafanyakazi kwa ujumla, wake kwa waume walikuwa wameshughulika na mazoezi ya onesho la mavazi, ndani ya vyumba mbalimbali vya jengo la ofisi za kampuni ya ADFC. Wanamitindo, wavulana na wasichana, wabunifu wa mavazi, wapiga picha za kawaida na za video, waongozaji filamu za matangazo ya biashara, ili mradi kila mmoja alionekana kuwa ndani ya shughuli nzito. Onespot alikuwa akipita sehemu zote hizo kukagua. Alipofika chumba alichokuwemo Vicky na Edo, aliongozana na mpiga picha wa kawaida. Alisimama nae akampa maagizo fulani ambayo hakuna aliyeyasikia kisha akaendelea kukagua vyumba vyingine kimojawapo kikiwa alichokuwemo Lulu na wafanyakazi wengine.
Vicky baada ya kuvaa gauni moja kati ya anayotakiwa ayavae siku ya maonesho, alijitokeza mbele ya Edo na kusema,
“Ëdo gauni hili naona ni jembamba mno sitakuwa na raha wakati wa kulivaa kwenye maonesho, linanibana.” Edo alipomuangalia aliona kuwa gauni hilo halina dalili zozote za kumbana, lakini amelivaa akiwa zipu ya nyuma mgongoni haikufunga.
“Lakini Vicky utasemaje gauni hilo linakubana wakati hata hujalivaa sawasawa? Hebu funga hiyo zipu kwanza tuone kama kweli linakubana”. Vicky alijipelekea mkono mgongoni bila kufanikiwa kuigusa zipu, ndipo alipomwendea Edo, kuacha wote waliokuwepo hapo, na kumwambia,
“Tafadhali Edo hebu nisaidie kuivuta hii zipu huku mgongoni kwangu.” Edo bila kutafakari hili wala lile alimwendea akasimama nyuma yake na kuifunga zipu ya gauni alilokuwa amevaa Vicky. Zoezi lilipoanza la kuoneshana na kuelekezana, kila kitu, Vicky alitaka apate uhakika toka kwa Edo. Mara kwa mara alimwendea na kumuuliza.
“Unaonaje Edo nikiwa nitapozi hivi au hivi.”
Wakati akisema hivyo huwa anamkaribia kabisa Edo kiasi cha kugusana nae, jambo ambalo Edo hakulipendelea, lakini hakuwa na la kufanya sababu walikuwa wamo ndani ya kazi tena mbele ya watu wengi tu.
Onespot baada ya mizunguko yake katika vyumba mbalimbali kukagua zoezi la onesho la mavazi linavyokwenda, mwisho alitia nanga katika chumba alichokuwemo Lulu na wenzake wengine wakifanya zoezi. Alivuta kiti pembeni mwa chumba hicho na kuketi juu yake. Alikaa kimya kwa kuuweka mguu wake wa kushoto juu ya mguu wa kulia na kuufanya mguu huo uning’inie. Kisha akaegesha uso wake juu ya kiganja chake cha kulia, alishika tama. Macho yake aliyaelekeza kwa Lulu tu, kila alilokuwa akifanya na kila alipozunguka ndani ya chumba hicho. Hapo awali Lulu aliona Onespot yupo katika ukaguzi wake wa kawaida, lakini baadae alihisi kuwa sio bure. Onespot ana lake jambo. Basi muda huo huo Lulu alianza kukosa raha. Alianza kukosea kosea au kurudia rudia kila alichoagizwa na kuelezwa kufanya na muongozaji wake, ambae mwisho ilibidi amuulize Lulu,
“Vipi Lulu! Umechoka au vipi?! Unaumwa?! Kwani nakuona mara moja umebadilika na sio makini tena kama kawaida yako!” Lulu alimuangalia Onespot huku uso kaukunja na kusema,
“ Hapana sina neno…Siumwi tuendelee tu.” Baada ya muda si mrefu yule mpiga picha aliyezungumza na Onespot bila kujulikana walilozungumza, alimjia tena pale alipokaa. Walizungumza tena, kisha mpiga picha yule nae akavuta kiti akakaa karibu na Onespot. Wote walikuwa wamemkazia macho zaidi, Lulu kuliko watu wote wengine waliokuwepo pale. Ilipotokea tena Lulu kubabaika katika
zoezi lake, Onespot alizuka kutoka pale kitini alipokuwa ameketi na kumwendea Lulu. Alipomfikia karibu alimkumbatia kwa nyuma kwa kushika mikono yake yote miwili na kuigandamiza tumboni kwa Lulu kwa kutumia mikono yake yeye Onespot, huku akiwa uso wake ameugusisha kabisa na wa Lulu. Kitendo hiki kilimfanya Lulu atulie na kuduwaa, maana hakukitegemea kabisa kama kingeweza kutokea. Alibaki kaduwaa kama sanamu bila kuchukua hatua yoyote kwanza. Onespot aliamka,
“Lulu…Lulu mbona hivyo, wewe ni mwanamitindo mzoefu na uliekwisha tengeneza na kuigiza filamu nyingi za matangazo kuliko wote hapa. Tena umeigiza na wanaume mbalimbali, sasa wasiwasi wako ni wa nini?!” Lulu kama aliyevumburuka kutoka usingizini ghafla alijitoa toka mikono ya Onespot kwa kutumia nguvu kidogo. Aligeuka na kutamani amnase kibao Onespot lakini akatanabahi kuwa wapo watu wengi mahali hapo wanaowaangalia. Alipata sababu hapo hapo ili kujitoa katika hali ya wasiwasi iliyotawala anga hizo, na kusema,
“Samahani waungwana, kusema kweli leo siko katika hali nzuri, ipasavyo.” Onespot pale pale alimwendea tena Lulu na kumshika bega lake la kulia kwa mkono wake wa kulia kupitia mgongoni kwa Lulu na la kushoto kwa mkono wa kushoto kama vile mtu anayomsaidia mgonjwa kutembea na akasema,
“Ah, aah! Takilifu ni ya nini Lulu?! Usijikalifishe…it is all right. Kama hujisikii vizuri twende nikusindikize nyumbani. Utaendelea na zoezi kesho when God wishes…We still have a time dear. Tunao muda mwingi wa kufanya mazoezi.” Wakati akisema hivi bado amemzuilia na anamuangalia usoni kwa jicho la huruma sana na kumjali. Lulu alitamani ardhi ipasuke na aingie, lakini hakuwa na la kufanya mbele ya macho ya watu wengi, isipokuwa kumuacha Onespot amuongoze kutoka pale chumbani. Walipofika kwenye ukumbi tu pasipokuwa na mtu, Lulu alimsukuma Onespot na kujitoa mikononi mwake. Alisimama mbele yake na kusema kwa sauti ya chuki.
“Hivi ni kwanini unanidhalilisha namna hii Onespot?!”
“Ni kwa sababu nina kupenda Lulu… I love you…I really do …dear!” Lulu aligeuka na kutaka kuondoka, bali Onespot alimshika mkono na kumgeuza amuangalie yeye.
“Unataka nini?!” Lulu alisema kwa ukali.
“Sema wewe unataka nini, nifanye, hata kama ni kukupigia magoti mbele ya watu mimi niko tayari.” Lulu alikuwa karibu chozi limtoke, alisema kwa taratibu kwa sauti ya kubembeleza.
“Tafadhali Onespot niache usinibughudhi…ndilo ninalolitaka, please, leave me alone… Hebu niache niwe huru.” Onespot nae alijifanya mnyonge ajabu na kumuulizia Lulu pasipo kumuangalia usoni, kwa sauti ya masikitiko.
“Ina maana… Lulu… Wewe ni mtumwa kwangu?!”
“La hasha… Mimi si mtumwa kwako, bali vitendo vyako kwangu, vinanifanya nikose uhuru ninaostahiki.”
“Ni vitendo gani hivyo Lulu? Unaweza kuniambia?!” Lulu alisimama hapa aliposimama huku akihema hema kwa chuki, kichwani mwake alifikiri aondoke au amuambie, mwisho aliona dawa ni kumwambia, alimtamka kwa haraka haraka,
“Vitendo vyako, kama ulinyofanya muda mchache uliopita vya kunikumbatia mbele za watu… ulikuwa una maana gani? Mimi ni nani wako? Ni mwanamke wako? Unafikiri watu watanielewa vipi? Usifikiri kuwa mimi ni msichana rahisi tu wa kukumbatiwa na kila mwanamme anaejihisi kufanya hivyo. Mwisho kabisa tendo la kuja nyumbani kwetu bila ya kualikwa. Kwa nini ufanye hivyo?!” Muda wote huu Onespot alimtulizia macho Lulu kwa kumuangalia na kumsikiliza kwa makini na huzuni usoni, baadae akajibu kwa sauti ya upole,
“Ni kwa sababu ya upendo Lulu, nakupenda. Naomba unisamehe kwa kila nililokukosea, si dhamira yangu kukudhalilisha. Love is blind you know, mapenzi ni
upofu. Apendae huwa anafanya mambo bila kuyaona kuwa ni mabaya. Niwie radhi Lulu, na ukubali kuwa yote niliyotenda ni kwasababu nakupenda mno.” Lulu alitulia na kumuangalia Onespot, kisha akatamka kwa sauti ya chini kumuuliza mvulana huyo,
“Lakini Onespot si nilikuambia kuwa sikupendi!”
“Pia uliniashiria kuwa unampenda Edward!”
“Kumbe unajua, Sasa?!”
“Ninatambua kwamba kukutaka kwangu hapo awali hakukuwa na mfuato mwema Lulu, my approach was not good. Nilijitapa mno, lakini baadae nilijua kuwa ninakupenda kweli, na kukuhurumia kuhusu huyo Edo wako!” Lulu alitoa macho kumsikiliza Onespot ambae alipofika hapo alisita kusema na kumuangalia Lulu.
“Mbona sikuelewi Onespot?”
“Edo ni ndumilakuwili”
“Eeeh, eti unasemaje?!!” Lulu alizidi kumkazia macho Onespot kwa shauku ya kutaka jibu.
“Ndio, Edo kakughilibu, wewe pamoja na Vicky.”
“Vicky?!”
“Vicky Kapate, katibu muhtasi wangu ni girlfriend wa Edo Oloi, na kila mfanyakazi hapa kwenye kampuni hii, analijua jambo hili isipokuwa wewe.” Onespot alimpa muda Lulu aimeze taarifa hiyo kwanza kabla ya kuendelea kusema,
“Kwa kuwa sasa hivi, Vicky nae ni mwanamitindo basi subiri utaona mwenyewe. Mimi ninakuambia hili tu sababu nakupenda. Nitasikitika sana nitakapokuona huna pakuegemea wakati Edo na Vicky watakapoamua kuwa wazi juu ya pendo lao jambo ambalo litakuwa hivi karibuni hali ya kuwa mimi nipo na ninakupenda kweli.” Lulu hakujua asema nini alibaki amesimama huku damu ikimwenda mbio ndani ya mwili wake. Onespot aliongeza kusema,
“Ninakuomba Lulu uniruhusu nikusindikize nyumbani japo kuwa mpaka nnje ya nyumba yenu tu, sawa?” Lulu bila kujijua alijisikia akitikisa kichwa kukubali na kutoa sauti ndogo ya chini.
“Sawa… Onespot.”
“Basi nisubiri hapo nnje ya ofisi” Onespot alimwendea yule mpiga picha aliekuwa amekaa nae. Kama kawaida yao wakaongea kidogo bila kusikika walichoongea, kisha akatoka na kumfuata Lulu aliekuwa nnje ya ofisi amesimama, anamsubiri. Alikata mitaa ya jiji la Dar es salaam taratibu, Onespot akiwa kimya nyuma ya usukani na Lulu nae akionekana ana mawazo kibao aliketi kwenye kiti cha kushoto mbele ya gari. Walipofika mbele ya nyumba aishio Lulu, Onespot aliliegesha gari mbele ya nyumba, akateremka haraka haraka, akazunguka na akaenda kumfungulia Lulu mlango wa gari. Baada ya Lulu kushuka, alimsimamisha mbele ya mlango huo wa gari, akamshika mabega yote mawili kwa mikono yake na kusema taratibu,
“Sikiliza Lulu, nakuomba usiamini maneno yangu moja kwa moja. Tumia macho yako vizuri utaona. Tumia masikio yako vizuri.. utasikia. Tumia kauli yako vizuri katika kuuliza utagundua na zaidi ya yote tumia akili yako katika kufikiri, lakini utambue kwamba hakuna mwizi anaeiba kisha akasema… hata mahakamani licha ya kuulizwa na mtu uraiani… kwa heri Lulu, nenda kapumzike tutaonana kesho.” Onespot alimuacha Lulu akivuta hatua kidogo kidogo kuelekea mlango wa mbele wa nyumba, alipoufikia karibu, nae aliingia ndani ya gari lake na kuondoka.
* * *
Kadri mazoezi yalivyoendelea kupamba moto ndivyo wakati wa kukutana Lulu na Edo ulivyokuwa mdogo au haupo. Kuonana kwao kulikuwa ni kwa
kusalimiana na kila mmoja kuelekea chumba chake cha kufanyia mazoezi. Edo yeye alikuwa akijipa matumaini kuwa baada ya onesho tu atamuuliza Lulu iwapo tayari amekwisha fikiria suala la ndoa na ikiwezekana wapange mipango yao. Edo alikuwa anampenda sana Lulu kwa wakati huu alijihisi. Lulu nae pamoja na hisia za pendo kubwa juu ya Edo, lakini tayari alianza kutia shaka ya kughilibiwa na wasiwasi juu ya uhusiano wa Vicky na Edo. Alianza kufarijika na maneno ya Onespot juu ya kuwa hakuamini kikamilifu, kwani wakati mwingi wa Onespot ulipotezwa kwenye mazoezi alipokuwemo Lulu. Ipo siku Edo alipatwa na udhuru wa kufiwa na jirani yao mtaa anaoishi. Habari hii alimueleza Vicky wakati wapo katika mazoezi.
“Samahani Vicky, leo itanibidi niondoke mapema ili nikawahi maziko ya jirani yetu.” Vicky hapo hapo aliwaza mbinu za kuitumia nafasi hiyo kufanikisha azimio lao. Alijidai kumshauri Edo kwa kusema,
“Unaonaje ukaenda kumfahamisha Onespot habari hii? Sababu akinikuta mimi nimekaa bure, itakuwa kero.” Edo alifikiri, kisha akaona si ushauri mbaya.
“Sasa sijui nitamuona wapi saa hizi!” Vicky alianza kucheka kwa nguvu kiasi cha kumfanya Edo ashangae.
“Mbona unanicheka Vicky?!”
“Hapana Edo sikucheki wewe, namcheka huyo Onespot!”
“Ana nini?!”
“Ah! Kwani siku hizi anabanduka chumba cha mazoezi cha Lulu! Nina hakika utamkuta huko huko!” Edo baada ya shughuli zake, alienda chumba alichokuwepo Lulu, kweli alimkua Onespot amekaa, na baada ya yeye Onespot kumuona Edo tu, alijifanya hakumuona na akawa anamwita Lulu.
“Lulu, Lulu?”
“Bee.”
“Hebu njoo mara moja.” Wakati Lulu anamwendea Onespot na Edo nae akamwendea huyo huyo. Kwa pamoja walifika mbele ya Onespot.
**ITAENDELEA..
TOA MAONI YAKO TAFADHALI!!
Comments
Post a Comment