Simulizi: Sitaisahau Tanga 17.
SITAISAHAU TANGA 17:
Nikawa natetemeka sana ndani ya ule mto na yule binti wa kitanga alizidi kunicheka pale juu.
Nikaanza tena kujitoa kwenye ule mto, nikajitahidi kutoa na kujikongoja tena hadi juu, nikawa namfata yule binti wa kitanga cha kustaajabisha akatoweka, nikaanza kuogopa na hofu kubwa ikanitanda moyoni. Mara mvua kubwa ya gafla ikaanza kunyesha, nikaamua kukimbilia mti uliokaribu ili nijikinge na ile mvua, nilipofika pale chini ya mti, mara upepo mkubwa ukaanza kuvuma na kusababisha ule mti kudondoka, nilitoka mbio na kuwa mbali na ule mti wakati unaanguka.
Mvua nayo iliendelea kunyesha tena kwa wingi kabisa, nikawa kama mnyama porini, nilitetemeka sana na hata nisijue cha kufanya kwani nilikuwa natembeatembea bila uelekeo wa maana, mvua iliendelea kunyesha na kufanya nizidi kutetemeka kwa baridi.
Mara gafla likaanza kuwaka jua kali sana tena lile jua la kuchoma utosini, nikazidi kushangaa na kustaajabu.
Mbele yangu ikatokea nyumba, nikaanza kujiuliza mbona ile nyumba sikuiona mwanzoni. Nikaamua kuisogelea ile nyuma na kujaribu kubisha hodi ila hakuna aliyeniitikia.
Nikaamua kuingia ndani hivyohivyo, nikakutana na mbibi akiwa anaota moto hata nikamshangaa kwa jua lile anaotaje moto, ikabidi nianze kwa kumsalimia
MIMI: Bibi shikamoo.
BIBI: Marahaba, nilijua tu ukiona nyumba utakuja.
MIMI: Na mbona unaota moto wakati kuna joto?
BIBI: Unajua mara nyingine inabidi tufanye vitu kinyume chake, usipende kuishi kwa mazoea.
MIMI: Kivipi bibi?
BIBI: Ndio kama hivi, mimi naota moto wakati ni joto. Wewe umezoea nini maishani?
MIMI: Nimezoea maisha ya kawaida bibi.
BIBI: Kwahiyo maisha unayoishi sasa ni ya kawaida?
MIMI: Hapana, naona majanga tu.
BIBI: Najua mambo yameenda kinyume, hukutarajia jambo hili. Ngoja nikwambie.
MIMI: Niambie bibi.
BIBI: Siku zote katika maisha unapofanya jambo kinyume huwa linaumiza wengine, au mimi sikuumizi wewe hapa ninavyoota moto wakati ni joto?
MIMI: Kweli naumia bibi.
BIBI: Basi unapofanya jambo kinyume na ukalizoea linakuwa kawaida ingawa linawaumiza wengine, ndio hivyo na wewe unapopatwa na kinyume cha uliyozoea lazima utaumia. Umejifunza nini hapo?
MIMI: Nimejifunza kuwa kinyume nilichofanya mazoea ndio kimekuwa kinyume changu sasa.
BIBI: (Akacheka), unapenda wasichana wazuri na wakuvutia, kila uwaonapo macho yako hayakuishi hamu. Mjukuu wangu, hii ni Tanga, mji mzuri wenye matunda ya kupendeza na mabinti wazuri.
MIMI: Unamaana gani bibi?
BIBI: Nina mabinti wengi sana tena ni wazuri sana kazi yao ni kuwapata vijana wenye tamaa kama nyie.
MIMI: (Nikiwa nimetoa mimacho tu), sielewi bibi.
BIBI: Damu za wengi zimekulilia wewe ila mabinti zangu wanafanya kazi nzuri sana kwani mwanaume yeyote mwenye tamaa kama yako awaonapo lazima ashtuke. Ngoja nikuitie watano uwaone.
Yule bibi akanyosha mkono juu kama ishara ya namba tano, mara wakatokea mabinti wazuri sana na wenye mvuto wa kipekee, nikabaki kuwaangalia tu.
BIBI: Unamtaka yupi kati yao?
MIMI: Hapana bibi sihitaji mwanamke yeyote.
Yule bibi na wale mabinti wote wakacheka sana halafu wale mabinti wakatoweka.
BIBI: Sogea karibu nami ili tuote moto vizuri, (huku akiendelea kuchochea kuni zake).
Nikawa nasita kuusogelea moto ule, akaniamuru tena nimsogelee pale. Duh kufika karibu ni kama jehanamu ndogo maana ule moto unaunguza taratibu mmh!! Yule bibi akaniangalia, yani ingawa ni mzee ila alionyesha kuwa na sura nzuri sana. Akaniuliza,
BIBI: Unajisikiaje sasa?
MIMI: Naungua bibi.
BIBI: Basi hii ni raha ya kufanya vitu kinyume mjukuu wangu.
Nikabaki nikimwangalia yule bibi na hata nisimmalize, mara akachukua glasi na kumimina kitu ndani yake na kunikabidhi,
BIBI: Karibu maziwa mjukuu wangu.
MIMI: (Nikapokea huku nikiangalia na kustaajabu), bibi mbona hii ni damu?
BIBI: Mbona unakuwa si muelewa mjukuu wangu? Nimekwambia kuwa hapa tunafanya vitu kinyume, sasa unashangaa nini kunywa!
Nikiwa bado nimeishika ile glasi na kuendelea kutafakari, mara yule bibi akasema,
BIBI: Na usistaajabu utakapotakiwa kutembelea kichwa badala ya miguu, (akacheka sana).
Bado nilikuwa kama mtu niliyepigwa na bumbuwazi bila ya kuwa na majibu na pale ule moto ulizidi kunichoma tu.
Mara yule bibi akainuka ila akawa anatembea kinyumenyume huku akicheka, na akarudi akitembea kinyumenyume vilevile.
BIBI: Hata ukitaka kuyarudia maisha ya kawaida utakubidi utembee kinyumenyume hadi utakapofika.
MIMI: Nionyeshe njia basi bibi.
BIBI: Kunywa maziwa kwanza.
Akatoa na bakuri na kunikabidhi,
BIBI: Tafuna na hizo karanga, ni tamu sana na hayo maziwa.
MIMI: Jamani bibi, mbona ni mavi ya mbuzi?
BIBI: Jifunze kuwa muelewa utashinda.
Nikawa nimeshika kile kibakuli chenye mavi ya mbuzi na ile glasi yenye damu hata nisielewe nakula vipi vitu hivi.
BIBI: Unapotumia kitu kinyume na wewe fanya kinyume chake utajikuta umekizoea na kuona cha kawaida.
MIMI: Jamani bibi, ndio nile mavi ya mbuzi na damu kweli?
BIBI: Bora ule maana nitakapokuletea maji ya kunywa hapa ushushie utakuwa umepata uzoefu kidogo.
MIMI: Khaaaa kama damu ndio maziwa na mavi ya mbuzi ndio karanga je hayo maji ni nini?
BIBI: (Akacheka sana), na hata nikikwambia hiyo damu ni damu gani utazidi kupagawa ni kheri ule ushibe hicho nilichokuandalia.
Bado maswali mengi yaliniandama, je hii damu ni damu ya nini? Bado sikupata jibu nikawa najipanga kumuuliza huyu bibi aniambie ukweli vyovyote vile sina jinsi.
MIMI: Samahani bibi, niambie hii ni damu ya nini?
BIBI: Unataka kujua kweli?
MIMI: Ndio nataka kujua bibi.
BIBI: Kunywa kwanza nikwambie.
Bado moyo wangu ulisita kunywa ile damu na kula yale mavi ya mbuzi.
ITAENDELEA

Comments
Post a Comment