HUBA – 4
Bwana Abed akakaa kwenye lile sofa nililokalia. Hapo macho yamenitoka dada namtazama huku nahema mpaka mapua yanachanua, nawaza mambo kumi kwa pamoja na katika hayo kumi tisa ni mabaya mno, nikawa nasubiri aongee tu nimlipukie kisawasawa ajute.
Basi naye akatulia tu kwanza yaani kama vile alikuwa anajua akianza kuongea tu na mimi nitaanza kubwabwaja. Unajua ile mtu anakutazama usoni moja kwa moja halafu kwa utulivu kabisa, nikapoa mwenyewe mpaka nikainamisha kichwa chini
Hapo ndiyo akanishika kidevu ile kurudisha uso wangu mbele yake, akanionyesha kwa kidole niutazame mdomo wake. Nikawa nafuata maelekezo. Akaniambia, Tulia. Jamani alitamka polepole kwa sauti ya kawaida akaniambia pale kwake hakuna sherehe, ila sherehe ipo *** kwa best yake. Kwa hiyo kama mpishi natakiwa nifikishe chakula kule shereheni
Nikaanza kupanik tena ile kusimama nimekunja uso nataka kumwambia hayo si makubaliano, akaniambia kaa chini mama kaa chini! Nikagoma akasimama akanirudisha kwenye sofa halafu nguvu ya kukataa sina, nikajikuta nimekaa tena.
Sasa akaniandikia kwenye simu, faida za kufikisha chakula kule kwenye sherehe yaani alinishawishi mpaka nikaona eeh kwani si binamu anajua likinikuta baya wataanza na yeye. Nikaomba nikabadili nguo, akasema sawa ila tunaondoka wote ananipitisha nyumbani kisha nikishabadili tunasepa. Eeh sawa? Mie sawaaa.
Kushika simu nakuta mafuriko ya meseji kutoka kwa binamu.Kufika nyumbani yuko juu juu ananiuliza kama nilikuwa kwa Abed au nilifikisha hotpot la mwisho nikaendelea na mambo yangu? Nikamdanganya hapo kisha nikamjuza nafikisha chakula kwenye sherehe yenyewe, akasema ooh twende wote.
Nikamwambia sawa maana nilihisi nikikataa mambo yatakuwa mengi, mama wakati huo hakuwepo alikuwa safari pale ndani mtu mzima alikuwa mamangu mdogo mgonjwa aagwe asiagwe hana shida. Pia dadangu mkubwa alikuwepo ila muda huo hakuwepo.
Kutoka tuko wawili,
Abed akashangaa alafu binamu mwenyewe akakaa mbele maana kamzoea bwana kuliko mie. Kweli tuliikuta sherehe nikamimina vyakula vyangu, tukakaa kidogo tu tukaondoka, sasa tumefika mie nimeshuka nimepeleka vyombo ndani binamu kakomalia siti ya mbele hashuki wanaongea tu. Hata kukawakatiza nikashindwa. Nikaingia zangu ndani.
Eeeh, binamu kutoka uko akaja kuniita eti Abed kasema mbona sijashukuru. Nikamwambia mlikuwa mnaongea ngoja niende nikamshukuru, binamu nae nyuma yangu kama kisigino. Nje hapo Abed kaegemea gari halafu hakukuwa na taa, sasa sie wenye masikio yenye shida na maongezi gizani ni maji na mafuta. Binamu akawa amesimama getini, mie nimemsogelea namwambia nashukuru bla bla bla yeye akijibu nasikia ghdegdhgdywgdjhg simwelewi hataaaa, nishajizoelea najibu sawa haya ili tu maongezi yaishe
Hapo tuliposimama naitikia ila mkono Abed ukawa umelifikia tumbo anatembeza vidole kutoka kitovuni kwenda kifuani, kuuchapa mkono autoe naona noma maana mfuma sweta yupo hapo nyuma, nikawa nabana pumzi alafu sielewi anaongea nini nasikia, “ so hakhshw malipo yakomjdhhghwgd ukipenda hdhdqjd eeoooii wewe dwdhwkhdwjh,” mimi naitikia sawaaa.
Mara binamu akasogea jamaa akaacha ujinga wakaongea binamu akanivutia ndani. Huko ndani ndio binamu akaniambia kasema malipo yako akutumie kwa simu au ufuate cash kesho, ila yeye binamu akasema atanichukulia hiyo kesho maana ataenda hapo kwake. Mie sawa. Niulize kama nililala sawasawa? Jamani nikigeuka nasikia msisimko kitovuni, mara namuota mara nashtuka mpaka kunakucha
Asubuhiiiii akapita nikaitwa kanipitishia hela yangu, akaniambia leta simu yako akasave namba yake akaandika vile vile My Husband Abed akanirudishia, nikamuuliza nini hiki eti nimemkunjia sura, akanisogelea ila karibu kabisa akatamka kitu flani kikaenda kusisimua mwili nikamsonya kujikaza tu, akacheeeka akaenda zake kwenye gari.
Sasa binamu anajikoki na madaftari nikamwambia hela nililetewa asubuhi, anashtuka wee saa ngapi? Nikamwambia asubuhi sana. Akaguna. Shing ngapi? Mie nikataja. Akashtuka kheee mbona nyingi hivyo? Nikamjibu mie sijui kanipa akaondoka. Nikaona mwenzangu uso unanyata. Sasa si alinitafutia tenda nami nipate senti? Sasa nimepata mbona tena uso wake unanyata?
Ikaanza hivyo, usiku meseji njwiii, ooh umelala? Siku imeendaje mama? Sijibu. Alikuwa ananiuliza sana kuhusu tatizo langu la masikio simuelezi chochote maana tangu nianze kuwaeleza hao wanaume sikuona mwenye kunielewa siku za mwanzo wanajifanya kujali baadae unaona kabisa anakuchoka, usiposikia basi hajiongezi. Hii kitu kwangu ilikuwa inaniumaaaa wala sitaki kudanganya nilikuwa strong
So the toxic me niliona haya ni maagizo matupu. Naogopa kabisa kuzoea huo upendo najua baada ya muda huyu akinikula tu yataanza yale mambo meusi ghafla unaambiwa niko busy sana, niko barabarani nikifika ntakucheki, unashangaa mtu anakaa barabarani siku tano utasema anaendesha lori la mpunga, hafiki, ukimtafuta anakwambia nimesafiri nikirudi fyoko fyoko fyoko, mnamaliza siku tatu kimya ukimcheki tu anajibu hapo hapo alikuwa busy, yaani ghafla mtu anajikuta wa maana sana kuliko pesa.
Ongeza huwezi kumpigia simu useme utampata haraka, unaandika meseji mpaka unafuta umejilalamisha yeye anakuchora tu tena anaweza kukushangaa ukimwambia unaumia coz meseji hajibu na kumpigia huwezi. Watu wanaotesa wenzao hivi Mungu asiwasahau kwenye mapigo 😭😭. Nikasema this time hakuna narcissist atanipata tena ataigiza mpaka apewe cheo cha Senior Master Lee Min Ho, kunguru wahed!
Siku hiyo akaniambia usipojibu hii meseji yangu nakuja saa moja jioni hapo kwenu utajua mwenyewe utanitambulishaje. Kwa kuwa naijua akili yake nikaijibu meseji aliyotuma ila nakiri kabisa sikuwa na majibu mazuri. Akaniambia kuna maongezi muhimu nichague nitafanyia getini kwetu au anikute mahali ama niende kwake. Tukajibizana hapo mwisho nikampa sharti ntakuja kwake na maongezi ni dakika 15. Ooh Laura makosaaaaa!
Yaani nilichomoka tu nyumbani nina dera langu moja hivi nimejitanda khanga mabegani, juu na mlemba wangu fresh, msimamo wangu siingii ndani nitakaa barazani. Akanigomea tukakaa sebuleni. Likaanza suala la kiburi. Akaniweka sawa. Hataki kujibiwa shit kama vile naongea na mtoto mdogo. Yeye ni mtu mzima na hajanivunjia heshima na zaidi ni mwanaume.
Akanitwanga, nahitaji heshima mama. Usinibwatukie kama tunasutana. Am your man Norat! Eti nikanywea. Akanitwanga tena, nataka ujue nakupenda halafu nakutaka. Na ujue najua wewe ni mtalaka, najua una mtoto, najua huna kazi, najua una shida ya masikio, lakini mimi nakupenda wewe Norat kama ulivyo hayo mambo mengine unayazingatia wewe sio mimi, so acha kunilisha fikra nisizonazo.
Mmmh nikagwaya, bwana nikaona ananishinda kwa hoja halafu kubwatuka siwezi. Nikamwambia bye bwana dakika 15 zimeisha nikasimama.
Ninachokumbuka nilikwenda mlangoni tukasimama hapo akaniambia nikivuka nikatoka hatokaa anisumbue tena, na kama kuna japo hisia za kumpenda na kujaribu kuona kama asemacho ni kweli, nimkumbatie. Mie tena nilitoka mpaka getini nikasimamaaa eeh nikarudi ndani, nikamkumbatia. Tulikaa hivyo kama dakika sijui, kukumbatia si kitu nilizoea ila kadiri muda ulivyokata niligundua ni kitu nilihitaji mno tena sana. Maana nilianza kulia. 😂😂
So we kissed , we hugged akaniruhusu kuondoka. Eeh nikaondoka nyie watu wazima buanaaa eeh niliondoka 😜
Ndiyo tukaanza hivyo mimi na Abed, mwenzangu hakutaka siri ila mi nilikuwa namhofia binamu. Mpaka siku moja akafuma meseji inaingia ina jina My Husband Abed. Kucheki namba ni za Abed. Wueeeh akacharuka akaniuliza kama nina mahusiano na Abed, nikamwambia ndio.
Nikaona machozi akashindwa kuongea tena wala hakujibu kitu ila nilijua nimemuumiza. Ukaribu kati yetu ulikufa kwa kipindi kirefu, nimekuja kuongea naye 2024 ni mimi nilimfuata nikamwomba msamaha kibinadamu najua mwenyewe wapi nilimkosea, i wanted peace between us maana katika watu ambao hawakuwahi kuninyanyapaa na walikuwa tayari kunisaidia huyu binamu yangu alikuwa mstari wa mbele kuliko hata mama yangu na dada yangu ambao waliosema maneno ya kuumiza juu yangu.
Nina mengi mengi ya kusimulia mengi sana, nifupishie na some details ziondoe kidogo. Niko na Abed mwaka wa sita sasa kama mke na mume, tuna mtoto mmoja, ndoa yangu haikuwa na sherehe coz nilikataa tu mwenyewe kuna mambo yalikuwa magumu nikaona isiwe tabu
Niseme nimepata mume ambaye shida yangu ya kusikia kwake si tatizo kabisa kabisa kabisaaaa, stress zilinipa maumivu ya miguu kuna muda niliumwa sana almost a year nilikuwa mtu wa kitandani tu after kujifungua, Abed ameniogesha, amenitunza kwa upendo mpaka nimekaa sawa.
Yeye ndio masikio yangu tukiwa public pamoja na haogopi wala haoni aibu, Laura kuna muda namuona kama sijui nini vile najiulize kitu gani kaona kwangu?
Imenichukua muda sana kurekebisha tabia zangu, hasira, ubabe, uchungu, mihemko, maneno ya kujihami na mengine yanayotokana na trauma. Abed ameninyoosha kisawasawa. Kunikosoa mimi ilikuwa kosa ujipange haswa la sivyo nalipuka na kujihami, saa hizi kukosolewa naona ni kurekebishana na kuelekezana. Amenivumilia mpaka sasa sina kelele Laura sinaaa, na ninaruhusiwa kuumia na kulalamika mtu akininyanyapaa kisha maisha yanaendelea.
Ukweni kwangu mie ni mzigo na wala hawakutaka ndugu yao aoe mtu kama mimi, Mungu mkali sana wifi yangu mtoto wake mkubwa wa miaka 15 kwa miaka miwili sasa ana shida ya masikio anahangaika na mashine za kila aina, maombi ya kila aina. Nipo hapa sishangalii ila walau wamepata jibu hii hali sio mkosi kama walivyoniita kama walivyonitenga kama walivyokuwa wananisema na kunicheka kisha yananifikia ni kitu kipo kinamfika yoyote
Abed na mimi tunagombana kama wenza wengine japo si mara nyingi coz Mungu amenipa mtu asiyejua kununa, asiyechoka kuandika kwenye karatasi, Norat i Love you mama usisahau kupitia dawa za mtoto. Haoni shida hata kuchat na mimi kwa simu na tupo wote hapo sebuleni, haoni shida kurudirudia maneno weee mpaka nielewe, haoni shida kujibu kwa niaba yangu tukienda sehemu ugenini tena anaweza sema wife hajakuelewa coz hajui Kiswahili heheheeee
Kanifundisha mpaka kusoma midomo yake tunaweza kuongea usijue nina tatizo coz naizoea sauti yake. Amenifanya nimekuwa submissive woman in a very romantic way kwa kweli, kuna muda namtoleaga sadaka tu huku machozi yananitoka maana kuna muda siamini ni mimi nina amani hivi
So, watu wa Mungu hivyo ulivyo kama atakupenda atakukubali hivyo ulivyo. Don’t settle for less kisa una ulemavu au hali fulani. Lakini pia hakikisha na wewe unapona majeraha ya trauma, wengi hatujui kuupokea upendo na kuutoa kwa shukrani ni process inayowataka wote muwe mmepona yaliyopita. Mie kwa kweli ningebaki nilivyokuwa kwa kuamini ndio kujiamini nisingekuwa na hii amani ya moyo na nisingekubali kuwa kuna sehemu nakosea pia.
Watu wa Mungu msiwaogope watu wenye kasoro fulani kama ulemavu. Mtu akimpenda mwenye hizo kasoro, ambazo wewe huziwezi usimvunje moyo au kumkejeli. Acheni hii tabia mnaumiza watu sana. Mnakosa utu, nimeliona hili sana kwangu wanasema yule kampendea nini mdada kama yule mara wanasema nitakuwa nna hela ndio maana mwanaume ananipenda sana, haloo kipato changu ni robo tu ya kipato cha hubby. Mtu akipendwa na kasoro zake tujifunze kuappreciate maana kesho zetu ni fumbo
Done! Nimemaliza Laura. Mwenye swali nitamjibu nikiweza. Yaani nikiwezaaaa. Sasa ngoja nikamtengee chakula My husband Abed!
_______________________
Mhusika amemaliza. Namshukuru mdau kwa muda wake. Ahsante pia kwa wasomaji kwa likes zenye kumpa motisha mleta Huba lake. Natumaini mmelifurahia.
