HUBA 03

ADMIN
0


 HUBA – 3


Nikatoka mpaka getini, nikamkuta bwana Abed na nguo zake smart, huulizi mara mbili kujua huyu bwana yuko njiani kwenda kazini, nikamuuliza enhee vipi tena? Mwenyewe anacheka tu, wasiwasi hana


Mie kwangu kulikuwa na mambo mawili, kwanza mama na mdomo wake, kila kukicha onyo lake lilikuwa nisimwongezee watoto waso na baba, pili  kuna huyo mfuma sweta na moyo wake, kila siku alikuwa anamwongelea Abed, leo kamsifia komwe kesho kamsifia sauti, mie kimya. 


Basi akanikumbusha aliniambia nisipoandika meseji kwake atakuja kugonga ndio kama hivyo kaja kweli. Nikamwambia nenda nitakutumia meseji akaenda zake, meseji nilokuja kumtumia nadhani hakuitarajia


Kwanza nilimkemea vikali sana, nilimpa yale mambo ya tuheshimiane naona huna adabu sipendi mambo ya kipumbavu sipendi utoto sipendi ujinga sipendi kuvunjiwa heshima kwani najiheshimu sana sijui umenionaje yaani nilijaza mineno mikali mikali nikamalizia na ukae ukijua mie mke wa mtu na nnajiheshimu sana unikome.


Sikujibiwaga hiyo meseji. Ikapita sijui wiki hivi akawa ananijia kichwani halafu ndio hatukutani nikarudia kuisoma ile meseji yangu roho ikaniambia mbona kama nilijibu vikali sana yaani vita ya fimbo mimi nimeenda kuchukua makombora ya nyuklia, akili ikaniambia mcheki ujifanye hata umekosea namba hivi ila nikaona utakuwa ujinga nikapotezea na namba nikafuta.


Sasa hapa nikwambie hayo majibu makali kipindi kile mtu angeniambia nna hasira za haraka, au nna majibu mabaya nisingekubali kabisa coz hizo hasira ndio nilikuwa naita kujiamini na hunibabaishi kitu, ukijichanganya nakukohoa, ikafanya niwe naogopwa uko nje,  yule dada kiziwi ila weee ana mdomo mkali hatari yote hii ilikuwa ni kujihami tu na sikujua naishi kwa kujihami  


Basi ikaisha kama wiki bilabila ajabu ndio akawa anakuja kichwani kwa fujo. Siku nilomuwaza sana ndio siku nilomwona dukani, alikuwa na mdada wakaingia kwenye gari wakaondoka, 


Kuna namna ka moyo kaliuma kidogo, nikajiambia ila huyu mkaka ndo walewale bora sikumsikiliza saa hizi ningekuwa naanza upya kuuguza moyo. 


Basi wiki nadhani iliisha sikumwona kabisa alafu kuna muda nilikuwa naenda tu dukani jioni ili sijui kumbahatisha  yaani kuna mahangaiko nilianza kuyapata hata mwenyewe sikuyaelewa, binamu akimtaja moyo unalipuka mradi tafrani


Siku hiyo jioni, nimefuata hela dukani kwa Mangi, nimesimama nasubiri Mangi amalize mahesabu yake Abed akafika pale dukani. Kile kitendo cha kusimama pembeni yangu nikahisi kama pumzi zinanikaba. Akaniinamia kidogo akanitazama usoni akaniambia nimekumiss. Nikamsikia. Nikajikaza ile kujikaza kwamba sitaki ujinga wake, nikamsonya nadhani na kumtazama vibaya kisha uso ukaelekea dukani najifanya namakinika na Mangi. Akaniandikia kwenye simu, hivi kosa langu nini mama?


Nikamgeukia hapo nikamtamkia mineno ya kukera haswa nilikwambia nilikuwa na mdomo mkali acha. Maana hapo nilimkumbuka yule mdada niliyemwona naye hapo dukani nikachefukwa. Najiuliza hivi ananionaje? Mtu mjinga au? 


Yeye sasa akaniangaliaaa akatabasamu akaagiza alichotaka dukani akaenda zake. yaani ile anaishia nafsi ikaanza kuniuma tena najiuliza sasa  sababu za kumropokea vile ni nini? Yaani ilibaki kidogo nimkimbizie nyuma ila nikajikaza najikumbusha wanaume sio watu kwani sijatosheka tu na kuumizwa? 


That day kiukweli nilihangaika , nikajilaumu tu sasa kwa nini nimemkaripia na kitu pekee kaka watu alifanya ni kunisalimia na kusema amenimiss. Hilo likapita, kama siku mbili hivi mfuma Sweta akaniambia kamaliza sweta lake anataka kumpelekea Abed, alafu anataka amsaidie masomo ya *** ambayo kipindi hiko binamu alikuwa anasoma chuo cha ***


Nikahisi moyo unavuta, najiuliza hiki ni nini. Mimi si simtaki huyu kaka sasa kwa nini naumia tena. Nikajiambia nipotezee tu hilo jambo ila nikawa nahisi kama kuna kitu kinaniponyoka, after all nilikuwa na ile hali ya kuamini na hivi nilivyo siwezi kuwa na thamani sawa na wenzangu wazuri wenye ukamilifu wa viungo, mwanaume gani atajisikia fahari kuwa na mimi? 


Nilikwambia niliingia kwenye mahusiano baada ya kuachika ila yakaishia pabaya, ni huyo mwanaume hakutaka watu wajue anatoka na mimi na nikaja kujua ananiponda kimtindo kwa wengine ndio maana alitaka mahusiano yawe ya siri, hii iliniuma sana so na huyu nikawa simwamini na nafasi simpi. 


Basi binamu alikuwa anaenda kusoma haswa wikendi, siku binamu akaja akaniambia Abed ana wageni siku fulani nimekuombea tenda ya vitafunio hiki na hiki na hiki, binamu akanitia moyo sana usilaze damu dada nakuamini, sasa kwa kuwa alinipa maelezo yote jumamosi hio nikajikoki miandazi michapati mikalmati, nikajaza hotpot zangu nikaanza kusomba moja moja napeleka.


Ndiyo mara ya kwanza kabisa kuingia ndani ya mji wake. Hiyo ni saa kumi na moja kasoro hivi mpaka namaliza hotpot la mwisho yeye amekaa kwenye sofa anaangalia TV sioni dalili ya wageni nikasema labda wa usiku. Nilipomaliza nikamjuza oda imekamilika, akasema poa.


Akainuka akafunga mlango mkubwa kwa ufunguo,  nikatoa macho. Akaniambia kaa hapo tuongee. Nikamwambia fungua mlango kwanza.  Akasema hafungui mpaka nishushe kiburi changu na kumsikiliza. 


Nikamwambia napiga kelele akasema piga tu, ila nikimaliza niweke matako chini tusikilizane na nimsikilize kama mwanaume mwenye akili timamu. Nikaleta zile za mie mke wa mtu, akanambia najua kila kitu kukuhusu, tulia hapo niongee.


Nikakaa chini, binamu akaniuliza kwa simu vipi mbona hurudi sherehe imeanza? Nikaanza kujibu Abed akachukua simu, akaiweka mbali.


Akakaa pembeni yangu kwenye sofa nililokaa.  Hapo moyo unakwenda mbio balaa. Binamu akaanza kunibeep, nikamwamabia walau ngoja nimjibu, akainuka akichukua ile simu akaisogeza sehemu ya chakula yaani mbali uko. Akarudi pembeni yangu.


Nikamwambia binamu atafikiria vibaya bure coz mi nilikuwa najua hisia za binamu kwake. Akanijibu fikra za binamu yako hazinihusu. Ninachotaka ni utulie hapo tuongee. Nikakosa pozi. 


ATAMALIZIA...

Tags

Post a Comment

0 Comments
Post a Comment (0)

Made with Love by

Pixy Newspaper 11 Template is Designed Theme for Giving Enhanced look Various Features are availabl…
To Top