RIWAYA: MUAFAKA - 7
MTUNZI: AMRI BAWJI SEHEMU YA SABA “Ujuzi wangu kama upi Onespot?!” Aliuliza. “Wewe u mpiga picha mzoefu na mwenye ujuzi na umekwisha fanya kazi hiyo na wanamitindo wengi wenye uzoefu, kwa hiyo utamuonesha Vicky staili zitakikanazo. Picha zake tutazihitaji kwa ajili ya matangazo ya biashara vile vile. Jambo hili ni muhimu kwa faida ya kampuni.” “Una uhakika kuwa sio kwa faida yako binafsi bosi Onespot?!” Edo aliuliza kwa dhihaka huku kimoyomoyo akiwa ni kweli analouliza. Onespot alicheka kwa nguvu huku akitikisa kichwa kukataa, “Hapana… hapana Edo… Oh no! sio kwa faida yangu binafsi… You must believe me Mr. Oloi.” Edo alielezwa nguo hiyo ambayo ataivaa Vicky ni lini italetwa na mara ifikapo zoezi lianze. * * * Wafanyakazi kwa ujumla, wake kwa waume walikuwa wameshughulika na mazoezi ya onesho la mavazi, ndani ya vyumba mbalimbali vya jengo la ofisi za kampuni ya ADFC. Wanamitindo, wavulana na wasichana, wabunifu wa mavazi, wapiga picha za kawaida na za video, waongozaji filamu za ...